Total Pageviews

Thursday, 31 December 2015

KILIMO CHA VITUNGUUMAJI

Vitunguu ni zao la mbogamboga na hulimwa kwa ajili ya balbu zake. Hulimwa nyanda za baridi kwa wingi sana.

Nyanda zenye joto vitunguu hulimwa pia. Tanzania vitunguu hulimwa sana sehemu za Mang’ula, Mgeta na Singida. Hata hivyo vitunguu hustawi maeneo mengi ya Tanzania.

Vitunguu vinaweza kulimwa mwaka mzima endapo maji yanapatikana.  Vitunguu vina matumizi mengi sana na vina madini joto,  chuma, vitamin A, vitamin B, vitamin C na vitamin E. 

HALI JOTO

Joto linatakiwa sana kwa ajili ya ukuaji wa balbu ila joto likizidi vitunguu hukomaa mapema kabla balbu hazijafikia ukubwa unaostahili, hivyo mkulima anaweza kupata mazao kidogo.

UDONGO NA MAHITAJI YA MAJI

Vitunguu huweza kupandwa kwenye udongo wowote wenye rutuba, usiotuamisha maji na usionata sana.  Hufanya vizuri kwenye udongo wenye asidi kidogo japo udongo wenye alkali kidogo sio mbaya sana. Kwenye udongo wenye mchanga mchanga umwagiliaji ni lazima. Udongo mzuri sana kwa ustawi wa vitunguu ni tifutifu-kichanga.

Umwagiliaji ni muhimu sana hasa wakati wa kuanza kutengeneza balbu. Unyevu uliozidi ni hatari sana kipindi cha ukuaji.

Epuka matumizi ya mbolea mbichi isioiva vizuri kwani husababisha vitunguu kuwa na shingo pana sana majani hukua sana badala ya balbu.

UZALISHAJI NA UPANDAJI WA VITUNGUU

Kabla ya kupanda udongo ni lazima utifuliwe vizuri na reki kuondoa mabaki ya mimea na mawe ama Vipande vikubwa vya udongo. Matuta yawe na upana wa mita moja. Vitunguu hupandwa kwa mstari mojakwamoja ama kutokea kitaluni. Pia huweza kupandwa kwa mstari pacha. Vitunguu hupandwa sm 10-15 kutoka mmea hadi mmea na sm 10-15 kutoka mstari hadi mstari.

EPUKA
Kununua mbegu za mitaani, kuzidisha sana mbolea na umwagiliaji usio na mpangilio kwani husababisha vitunguu kuzaa pacha.

Pia epuka kupanda vitunguu mahali palipopandwa mboga jamii ya vitunguu siku za nyuma. Mfano Vitunguu saumu na vitunguu majani.

KITALU CHA VITUNGUU

Ni muhimu kumwagilia maji ya kutosha siku kumi za mwanzo tangu kusia mbegu kitaluni. Vitunguu hukaa kitaluni kwa wiki 6-8 na miche ifikiapo upana wa penseli na urefu wa sm 15 ni tayari kwa kuhamishia shambani/bustanini.

AINA ZA VITUNGUU VINAVYOLIMWA TANZANIA
.  Red Creole
.  Bombay Red
.  Hybrid F1

UTUNZAJI WA SHAMBA

Kutandazia shamba na majani yaliyooza vizuri ama mabua inashauriwa ili kuongeza ruba ya ardhi, zuia magonjwa yatokanayo na udongo na magugu. Kupanda vitunguu kwenye matuta yaliyoinuka ni muhimu sana kuzuiya utuamishaji wa maji na mlipuko wa magojwa ya miche. Kungoa magugu na uvunaji ufanywe kwa mkono.

MAHITAJI YA MBOLEA

Vitunguu hufanya vizuri kama shamba litawekewa mbolea ya samadi ama mboji ilioiva vizuri. Kiasi cha tani 25-40 kwa heka kinashauriwa. Hii ni sawa na kilo 7.5 -12 kwa tuta lenye urefu wa mita 3 na upana wa mita 1.

UVUNAJI

Vitunguu huvunwa kuanzia siku 90-150 tangu kusia mbegu. Dalili za kukomaa ni kuanguka kwa majani.

Vitunguu huvunwa kwa kuvuta kwa mkono na kuhifadhiwa siku kadhaa shambani vikiwa vimefunikwa na majani. Baada ya hapo majani hukatwa na balbu hupakiwa kwa ajili ya kuhifadhi kusubiria bei nzuri. Vitunguu huweza kuhifadhiwa hadi miezi 9 tangu vivunwe bila kuharibika. Vitunguu vihifadhiwe kwenye nyuzijoto chini ya 4.4 °C ama juu ya nyuzijoto 25°C ili visiharibike.

UUZAJI

Vitunguu ni zao lenye bei nzuri ukilinganisha na mazao mengine ya mbogamboga na huuzwa kwenye masoko ya kawaida kwa bei nzuri. Kwa hivi sasa (sep. 10) hapa Morogoro vitunguu kilo moja ni Tshs. 1500/=. Kama vitunguu vikilimwa vizuri na kuhudumiwa ipasavyo Ekari moja huzaa gunia 70- 90 sawa na kg 7,000-9,000. Kama akipata soko la uhakika mkulima anaweza kupata hadi 13.5 milioni kwa msimu mmoja.








No comments:

Post a Comment