Tuta absoluta (nondo) wanataga
mayai usiku kwenye sehemu ya juu
ya mimea, kwenye sehemu ya chini ya
majani au shina changa au sehemu za
maua. Katika maisha yao, mdudu jike
huweza kutaga hadi mayai 260.
Wakulima wa nyanya nchini Tanzania
na maeneo jirani, wameingiwa na hofu
kubwa baada ya kuenea kwa haraka
mdudu hatari anaeangamiza zao la
nyanya.
Mdudu huyo anayejulikana kama
nondo wa nyanya, na kitaalamu Tuta
absoluta, aligundulika kuwepo nchini
tangu mwaka 2014, lakini madhara
yake yameanza kuonekana zaidi
mwaka huu na anaathiri uzalishaji wa
nyanya kwa kasi na kiasi kikubwa sana
jambo lilopelekea wakulima kumbambika
jina la “kanitangaze”.
Ni muhimu kwa wakulima kumtofautisha
mdudu huyu na yule mwenye
mapindo, ambae kwa kawaida hushambulia
nyanya na mazao mengine.
Wadudu wenye mapindo ni aina ya
inzi-buu lake huzalisha kijumba chembamba,
ambacho husukwa kwenye
majani, lakini hakishambulii tunda
kama ilivyo kwa Tuta absoluta.
Tuta absoluta ni nondo na buu lake
huzalisha vijumba vikubwa, ambavyo
hushambulia tunda la nyanya na
hatimae kusababisha hasara kubwa
kwa mkulima.
Tabia za wadudu hawa
Wadudu wakubwa wanafanya kazi
usiku na mapema wakati wa asubuhi.
Majira ya saa 1 hadi 5 asubuhi
wanaweza kuonekana wakiruka
kwenye sehemu ya juu ya mmea.
Muda unaobaki wa siku wanajificha
kwenye sehemu ya chini ya majani.
Kwa kawaida huwa wanataga
mayai usiku kwenye sehemu ya juu
ya mimea, kwenye sehemu ya chini ya
majani au shina changa au sehemu za
maua. Katika maisha yao, mdudu jike
huweza kutaga hadi mayai 260.
Mayai yanapoanguliwa, mabuu
hutumia masaa machache kujilisha juu
ya mmea. Baada ya hapo, wanaingia
ndani yam mea ambapo hukaa hadi
wapevuke na kuwa wadudu wakubwa.
Baadhi ya mabuu walio kwenye
mabadiliko huondoka kwenye pango
walilopo na kuanzisha jingine, wakati
mwingine ni ndani ya tunda. Buu
mmoja linaweza kuharibu tunda
zima kwenye shada. Wakati mabuu
wanapozunguka mmea, wanafanya
haraka sana kwa msaada wa nyuzi
nyororo walizotengeneza.
Ukuaji
Ukuaji wa buu hufanyika kwenye
udongo na kwenye mimea yenyewe.
Mdudu anapopevukia kwenye mmea, hutengeneza kijumba chenye nyuzi
laini ili kujilinda. Tuta absoluta ana
uwezo wa kuwa na vizazi vingi katika
kipindi cha miezi 12. Katika maeneo
yenye joto, mzunguko unaweza kukamilika
chini ya mwezi mmoja.
Kutokana na muda wa mzunguko
wa maisha kuwa mfupi, kuna hatua
nyingi za mdudu huyu kuharibu
mmea kwa kila kipindi kimoja cha
maisha yake.
Wadudu hawa hawapendi baridi
kali wala joto kali sana. Chini ya nyuzi
joto 10 inazuia ukuaji wa mdudu huyu,
na zaidi ya nyuzi joto 30 hufa.
Uharibifu
Wadudu hawa husababisha uharibifu
enezi wa jani pamoja na tunda, ambao
unaweza kusababisha hasara ya asilimia
100 kwa mkulima. Mimea ya
nyanya inashambuliwa kuanzia hatua
za awali, hadi inapotoa matunda.
Uharibifu wa awali hupelekea hatua
ya pili ya maambukizi ya kuvu na
bakteria.
Buu linaweza kushambulia tunda
mara tu linapotengenezwa. Huharibu
pia vichipukizi ambavyo husababisha
ukuaji mbovu wa mmea.
Udhibiti
Kwa kawaida utunzaji wote wa mazao
hutegemea maamuzi madhubuti
na utunzaji sahihi wa shamba. Kwa
upande wa utunzaji wa mazao, mdudu
mharibifu anatakiwa asipate chakula
kwenye mmea unaomhifadhi.
Ili kudhibiti wadudu hawa,
zingatia mambo muhimu
yafuatayo:
• Usipande tena mazao hifadhi mara
tu baada ya uzalishaji wa mazao
hifadhi ya mwanzo.
• Rudia kupanda mazao yasiyokuwa
jamii ya mnavu
• Unaweza kuacha eneo hilo kwa
muda wa wiki 5 hadi 6 bila kuwa na mimea hifadhi. Hali hiyo itasaidia
kuondoa kizazi cha wadudu hao katika
eneo hilo
• Ondoa magugu yote yenye majani
mapana. Weka mkazo kwenye
kuondoa magugu jamii ya mnavu
• Ondoa mara moja masalia ya mazao
ya zamani, kisha yafukie
• Ondoa nyanya zilizoharibiwa
kutoka kwenye mmea na uziteketeze
• Kuwa makini na utendaji wa majirani
katika mashamba yao
• Pangilia eneo lako vizuri kwa
kuweka nafasi kutoka katika shamba
la jirani
Shughuli za binadamu
Mdudu huyu anasambaa kwa haraka
sana kutokana na shughuli za binadamu.
Ni muhimu kufanya juhudi ili
kuzuia uenezaji unaotokana na shughuli
hizo.
Tuta absoluta wanaweza kutaga
mayai kwenye miche iliyopo kwenye
kitalu. Hivyo kabla ya kutoa miche
kwenye kitalu ni lazima ichunguzwe
kwa umakini, ili kuona kama kuna
dalili za wadudu waharibifu.
Endapo wafanyakazi wamekuwa
kwenye shamba lililozagaa wadudu,
ni muhimu kuhakikisha kuwa hawabebi
wadudu kwenye nguo zao kutoka
eneo moja kwenda lingine.
Hakikisha kuwa hakuna tunda
lililoathiriwa na mdudu linalopelekwa
sokoni. Tunda lililoharibika
liteketezwe.
Vikapu na matenga yanayotumika
kuvunia kwenye eneo lililoathirika,
visipelekwe kwenye eneo safi ambalo
halijaathiriwa.
Viuatilifu
Kuna aina nyingi za viuatilifu vinavyoweza
kuua aina hii ya wadudu-
“Tuta absoluta” lakini kuna mambo
mengi yanayowasaidia wasife kwa
urahisi.
• “Kanitangaze” Tuta absoluta, hujificha
wakati wote. Anapokuwa
mkomavu hujificha chini ya majani
au mabuu ndani ya majani au tunda.
Hali hii hufanya viuatilifu vya mguso
au kunyunyiziwa kushindwa kuleta
mafanikio.
• Mdudu huyu hujenga uwezo wa
kushindana na dawa zilizotumiwa
kupita kipimo.
Ili kuweza kukabiliana na mdudu
huyu, ni muhimu sana kutumia kiasi
kidogo sana cha viuatilifu kwa kuwa
wana uwezo wa kujenga usugu kukabiliana
na dawa hizo. Au kutumia
dawa za asili zinazoaminika kuwa na
uwezo wa kukabiliana na aina hiyo ya
wadudu.
No comments:
Post a Comment