Total Pageviews

Wednesday, 3 February 2016

Kilimo cha Maua



Ndugu Wapetani, kuna haja kubwa sana kwetu kuwa wabunifu na kuweza kuifanya biashara yetu hii kuwa yenye mvuto na tija kwetu.  Nasema haya kwa kuwa tumekuwa kama tumejisahau kidogo kwa kukaa na kusubiri wateja waje katika maeneo ya biashara zetu ili kutupa mia mbili mia tatu, tuna ishusha thamani biashara hii.  Hebu tutafute njia ya kulipendezesha jiji kwa kuingia mikataba maeneo mengi kwa ku design maeneo mengi na kuweka maua pamoja na miti,  tuandike miradi yetu na kuweka faida za kuwa na bidhaa zetu katika jiji hili la Dar es Salaam na Wilaya zake, tuwabadili fikra wakazi wa Dar kwa kuwa wekea mazingira mazur na si mabiwi ya takataka tunazoona na harufu mbaya tunayoinusa kila kukicha.  Ni wakati sasa wa kubadilika na kulitengeneza jiji.

Hivi ni lini mara ya mwisho umewaona vipepeo wazuri katika macho yako wakikatisha mbele ya macho yako zaidi ya inzi wa aina mbili, kama sio yule wa chooni , basi yule wa majalalani na katika vidonda na vinyesi anayetuletea magonjwa kama kipindupindu na maradhi mengine ya kijingajinga.

Tutumie fursa hii sasa ili kujiingizia kipato lakini pia kulipendezesha jiji.

Jiji la Dar tunaambiwa hakuna mashamba lakini tunaweza kuwa na mashamba ya maua na kuzalisha ajira kwa kulima, kuhifadhi na kuuza maua bila ya kuharibu taratibu za jiji.

Hii ni njia nzuri ya kuwavutia hata wadau na kuanza kuifanya hii biashara kuwa ajira, tena ajira yenye tija kwa wakulima kufanya biashara ndani na nje ya nchi.




Tuchukue mfano wa majirani zetu Kenya wao inakadiriwa zaidi ya Wakenya 500,000 wamejiajiri katika biashara hii, na wameajiri zaidi ya wafanyakazi 90,000 katika mashamba yao.

Mwaka 2013 tani zipatazo 125,000 za maua zilisafirishwa nje ya nchi na kuwaingizia kiasi cha dola za kimarekani 507 milioni ( kiasi cha shilingi za kitanzania 1,110,330,000,000/=) (Trilioni 1.1).

Kiasi cha 25.3% ya pato la Kenya hutokana na kilimo kwa ujumla, na kilimo cha maua kinachangia 1.3%

Wenzetu wakenya 35% ya maua, wanauza ulaya hasa nchi za Holland, Germany, UK, na nyinginezo.  Pia Kenya wana mashamba 127 yanayotambulika na kufanya biashara kimataifa.

Ni wajibu wetu wafanyabiashara wa kilimo hiki tuwe wbunifu na tushirikiane katika kuleta maendeleo yetu binafsi na ya taifa kwa ujumla.  Ukilitenga taifa kwa kutaka biashara iwe yako kama kisiwa hutapiga hatua zaidi ya kuishia kulaumu na kuona kama vile hii sio ajira yenye kuhitaji kulipwa mshahara mnono.

Twaweza jadiliana kwa wale wanaotaka tujiunge kwa pamoja na kuifanya biashara hii kuwa ajira rasmi itakayotuingizia kipato kikubwa kwetu na kwa taifa.  Jiunge nami kwa  WhatsApp namba +255765903379 FREBU Farm Group

JINSI YA KULIMA UYOGA NYUMBANI







Kabla ya kuzalisha uyoga inabidi kuwa na chumba chenye paa ambalo litazuia jua, mvua na vumbi.
Chumba hiki kinatakiwa kiwe na sakafu inayohifadhi unyevunyevu pamoja na sehemu ya giza ambayo ni muhimu kwa kuotesha utandoa wa Uyoga. Mkulima wa kawaida anaweza kutumia kasha kama sehemu ya giza.
Hatua muhimu katika kuotesha Uyoga baada ya kupata mbegu ni kama ifuatavyo;
Kusanya masalia ya mazao kama vile mabua, majani ya mpunga, ngano, pumba za mpunga au mahindi, masalia ya miwa baada ya kukamua n.k. Vitu hivi hutumika kama mali ghafi kwa kuoteshea Uyoga. Mabua, Majani ya Mpunga au Migomba yakatwe kwa urefu usiozidi sentimeta 6, au urefu wa vidole kwa kutumia panga au kisu.
Loweka mali ghafi kwenye maji ya kawaida kwa muda wa siku nzima ( saa 24). Kisha yachemshwe kwa muda wa saa 2 ili kuua vijidudu pamoja na vimelea vilivyomo. Ipua na umwage maji yote halafu tandaza kwenye kichanja kisafi ili yapoe bila kuchafuliwa na vumbi au vijidudu. Kisha jaza mali ghafi hii katika mifuko ya nailoni tayari kwa kupanda mbegu. 
Namna ya kupanda.
Kuna aina mbili za upandaji;

AINA YA KWANZA
Chukua mfuko wa nailoni, weka tabaka ya mali ghafi ya kuoteshea kiasi katika mfuko halafu tawanya mbegu juu yake. Baada ya kuweka mbegu, weka tena tabaka nyingine ya kuoteshea na kuweka mbegu juu yake.

Endelea kuongeza tabaka kwa namna hii mpaka ifikie ujazo wa robo tatu ya mfuko.
NB: Tabaka la mwisho la juu lazima liwe la vioteshea.

AINA YA PILI
Changanya mali ghafi ya kuoteshea ( baada ya kuchemsha na kupoa) na mbegu ya uyoga katika uwiano wa 1:25 ( mbegu : mali ghafi ya kuoteshea).Kwa uyoga aina ya Mamama (Pleurotus spp), kisha mchanganyiko huu ujazwe katika mifuko ya nailoni.

Mifuko hii iwe ya ukubwa wa sm 20 kwa sm 40 ambamo unaweza kujaza kilo 1-1.5 ya mali ghafi ya kutosha. Katika njia zote mbili, funga mifuko na toboa matundu kwenye mifuko yenye kipenyo cha sm 6 hadi 10 kwa kila mfuko. Zingatia:
(i) Matundu yawe mengi ili kuingiza hewa ya kutosha ndani ya mifuko.
Uyoga ni Kiumbe hai, hivyo unahitaji kupumua.
(ii) Ukishanunua mbegu, kama hupandi kwa muda huo, hifadhi kwenye jokofu. Kama huna jokofu, nunua mbegu baada ya kuandaa kila kitu.
Mbegu za uyoga zinaweza kuota vizuri hata zikikaa nje ya jokofu kwa siku mbili.
(iii) Waweza kutumia chupa moja yenye ujazo wa mililita 300 kwenye kilo 15 za mali ghafi ya kupteshea.
Hakikisha unamaliza mbegu yote kwenye chupa kwani ikibaki itapata maambukizo ya vimelea.
(iv) Hakikisha unaponunua mbegu iwe ni nyeupe. Mbegu ambayo siyo nyeupe ni dalili za maambukizo ya vimelea. Vingine na hivyo haifai kupandwa .

MATUNZO YA ZAO LA UYOGA.
Weka mifuko kwenye chumba cha giza. Kwa mkulima wa kawaida waweza kutumia kasha lisilopitisha mwanga kama chumba cha giza. Acha mifuko humo kwa muda wa siku 14-21 bila kufunua ili ukungu mweupe uweze kutanda vizuri. Utando wa uyoga ukishatanda vizuri kwenye mali ghafi ya kuoteshea, hamishia kwenye chumba cha mwanga na hewa ya kutosha kisichopigwa jua.
Katika chumba chenye mwanga. Mifuko inaweza kuwekwa kwenye meza, chanja ya waya au miti.
Mifuko pia inaweza kuning'inizwa kwenye kamba.

NB: Unaweza kunyunyizia maji juu ya mifuko yaliyochemshwa na kupoa, mara tatu au zaidi kwa siku.

Tahadhari: Usizidishe maji kwani maji yakiwa mengi sana yanaweza kuozesha uyoga.

Aina nyingi za uyoga huanza kutoa vichwa siku 2-3 baada ya kuwekwa kwenye mwanga.

UVUNAJI WA UYOGA.
Uyoga huwa tayari kuvunwa siku tatu baada ya vichwa kuonekana. Uyoga uvunwe kwa mkono kwa kushika katikati ya shina la uyoga, kisha zungusha hadi uyoga ung'oke. Usiondoe kichwa peke yake katika kuvuna uyoga kwa kubakiza shina huzuia uyoga mwingine kutokea.

Nakutakia mafanikio katika kilimo 

Je Wajua kuwa Uyoga ni Kinga ya Saratani?
Uyoga una vitamini na aina nyingi za madini.
Virutubisho vilivyothibitishwa kuwemo kwenye uyoga ni pamoja na Vitamin B2, B3, B5, B6, B Complex pamoja na madini ya Potasiamu na ‘phosphorus’.
Virutubisho hivyo ni muhimu
kwenye mwili wa binadamu katika kutoa na kuimarisha kinga ya kupambana na ‘wavamizi’ maradhi.
Aidha,
inaelezwa kuwa uyoga ni chanzo kingine kizuri sana cha madini ya chuma (iron) na kopa ambayo yanahusika kwa kiasi kikubwa na uwezeshaji wa usambaza wa hewa ya oksijeni mwilini. Kupatikana kwa madini ya chuma na kopa kwenye uyoga ni jambo la kipekee ambalo linafanya mmea huo kuwa tofauti na muhimu.
Nguvu za uyoga 
(Mashrooms) kwa mapana, inaelezwa kuwa Vitamin B2 inayopatikana kwenye uyoga, ni tiba tosha kwa watu wanaosumbuliwa na ugonjwa wa kichwa unaojulikana kama ‘kipanda uso’. Kiasi kidogo cha uyoga utakachokula kitapunguza kasi ya kuumwa kichwa hicho.
Vitamin B
inasifika kwa uwezo wake wa kuzuia uchovu wa mwili (fatique) na akili hasa wakati wa kazi nyingi. Vitamin B3 husaidia kupunguza kiwango cha mafuta mabaya ya Lehemu mwilini, wakati Vitamin B6 yenyewe huondoa hatari ya mtu kupatwa na kiharusi au moyo kusimama ghafla (Heart Attack).
Faida za kiafya zilizo orodheshwa hapo juu zinazopatikana kwenye uyoga hazikutosha, basi kuna faida nyingine ambayo inatokana na madini aina ya Zinc yanayopatikana kwa wingi kwenye mboga hii. Zinc ina faida nyingi sana mwilini na miongoni mwa faida hizo ni uimarishaji wa kinga ya mwili (Immune System).
Zinc si muhimu tu kwa uimarishaji wa kinga mwilini, bali pia kwa uponyaji wa haraka wa vidonda mwilini. Vilevile mboga hii inasaidia sana ukuaji mzuri wa seli za mwili, huimarisha kiwango cha sukari mwilini na kukufanya kusikia ladha na harufu ya vyakula na vitu vingine ipasavyo.
Kwa ujumla uyoga ni mboga muhimu na inapaswa kuliwa na kila mtu anayejali afya yake kutokana na faida zinazopatikana humo. Kuanzia leo, jaribu kuweka uyoga katika orodha ya mboga unazonunua kila wiki kwa ajili ya familia yako.


Thursday, 31 December 2015

KILIMO CHA VITUNGUUMAJI

Vitunguu ni zao la mbogamboga na hulimwa kwa ajili ya balbu zake. Hulimwa nyanda za baridi kwa wingi sana.

Nyanda zenye joto vitunguu hulimwa pia. Tanzania vitunguu hulimwa sana sehemu za Mang’ula, Mgeta na Singida. Hata hivyo vitunguu hustawi maeneo mengi ya Tanzania.

Vitunguu vinaweza kulimwa mwaka mzima endapo maji yanapatikana.  Vitunguu vina matumizi mengi sana na vina madini joto,  chuma, vitamin A, vitamin B, vitamin C na vitamin E. 

HALI JOTO

Joto linatakiwa sana kwa ajili ya ukuaji wa balbu ila joto likizidi vitunguu hukomaa mapema kabla balbu hazijafikia ukubwa unaostahili, hivyo mkulima anaweza kupata mazao kidogo.

UDONGO NA MAHITAJI YA MAJI

Vitunguu huweza kupandwa kwenye udongo wowote wenye rutuba, usiotuamisha maji na usionata sana.  Hufanya vizuri kwenye udongo wenye asidi kidogo japo udongo wenye alkali kidogo sio mbaya sana. Kwenye udongo wenye mchanga mchanga umwagiliaji ni lazima. Udongo mzuri sana kwa ustawi wa vitunguu ni tifutifu-kichanga.

Umwagiliaji ni muhimu sana hasa wakati wa kuanza kutengeneza balbu. Unyevu uliozidi ni hatari sana kipindi cha ukuaji.

Epuka matumizi ya mbolea mbichi isioiva vizuri kwani husababisha vitunguu kuwa na shingo pana sana majani hukua sana badala ya balbu.

UZALISHAJI NA UPANDAJI WA VITUNGUU

Kabla ya kupanda udongo ni lazima utifuliwe vizuri na reki kuondoa mabaki ya mimea na mawe ama Vipande vikubwa vya udongo. Matuta yawe na upana wa mita moja. Vitunguu hupandwa kwa mstari mojakwamoja ama kutokea kitaluni. Pia huweza kupandwa kwa mstari pacha. Vitunguu hupandwa sm 10-15 kutoka mmea hadi mmea na sm 10-15 kutoka mstari hadi mstari.

EPUKA
Kununua mbegu za mitaani, kuzidisha sana mbolea na umwagiliaji usio na mpangilio kwani husababisha vitunguu kuzaa pacha.

Pia epuka kupanda vitunguu mahali palipopandwa mboga jamii ya vitunguu siku za nyuma. Mfano Vitunguu saumu na vitunguu majani.

KITALU CHA VITUNGUU

Ni muhimu kumwagilia maji ya kutosha siku kumi za mwanzo tangu kusia mbegu kitaluni. Vitunguu hukaa kitaluni kwa wiki 6-8 na miche ifikiapo upana wa penseli na urefu wa sm 15 ni tayari kwa kuhamishia shambani/bustanini.

AINA ZA VITUNGUU VINAVYOLIMWA TANZANIA
.  Red Creole
.  Bombay Red
.  Hybrid F1

UTUNZAJI WA SHAMBA

Kutandazia shamba na majani yaliyooza vizuri ama mabua inashauriwa ili kuongeza ruba ya ardhi, zuia magonjwa yatokanayo na udongo na magugu. Kupanda vitunguu kwenye matuta yaliyoinuka ni muhimu sana kuzuiya utuamishaji wa maji na mlipuko wa magojwa ya miche. Kungoa magugu na uvunaji ufanywe kwa mkono.

MAHITAJI YA MBOLEA

Vitunguu hufanya vizuri kama shamba litawekewa mbolea ya samadi ama mboji ilioiva vizuri. Kiasi cha tani 25-40 kwa heka kinashauriwa. Hii ni sawa na kilo 7.5 -12 kwa tuta lenye urefu wa mita 3 na upana wa mita 1.

UVUNAJI

Vitunguu huvunwa kuanzia siku 90-150 tangu kusia mbegu. Dalili za kukomaa ni kuanguka kwa majani.

Vitunguu huvunwa kwa kuvuta kwa mkono na kuhifadhiwa siku kadhaa shambani vikiwa vimefunikwa na majani. Baada ya hapo majani hukatwa na balbu hupakiwa kwa ajili ya kuhifadhi kusubiria bei nzuri. Vitunguu huweza kuhifadhiwa hadi miezi 9 tangu vivunwe bila kuharibika. Vitunguu vihifadhiwe kwenye nyuzijoto chini ya 4.4 °C ama juu ya nyuzijoto 25°C ili visiharibike.

UUZAJI

Vitunguu ni zao lenye bei nzuri ukilinganisha na mazao mengine ya mbogamboga na huuzwa kwenye masoko ya kawaida kwa bei nzuri. Kwa hivi sasa (sep. 10) hapa Morogoro vitunguu kilo moja ni Tshs. 1500/=. Kama vitunguu vikilimwa vizuri na kuhudumiwa ipasavyo Ekari moja huzaa gunia 70- 90 sawa na kg 7,000-9,000. Kama akipata soko la uhakika mkulima anaweza kupata hadi 13.5 milioni kwa msimu mmoja.








Wednesday, 23 December 2015

Bilinganya Nyeupe

Zao lenye pato kubwa



Bilinganya nyeupe (Long White Eggplant) ni moja ya zao la mbogamboga ambalo lina viini lishe vingi na muhimu kama vile madini aina ya chokaa na chuma, Vitamini A, B na C, wanga, protini na maji

Kisayansi zao hili hujulikana kama Solanum Melongenai na kilimo chake huweza kufanyika katika majira yote ya mwaka.

Hali ya Hewa
Zao hili huhitaji hali ya joto la wastani, udongo wenye kina kirefu na rutuba ya kutosha na usiotuamisha maji. Kwa kawaida bilinganya hulimwa zaidi ya msimu mmoja, lakini katika nchi za kitropiki (joto) zao hili hulimwa kwa msimu mmoja.

Udongo
Zao la hili huota katika udongo wa kichanga na tifutifu, wenye rutuba ya kutosha. Unashauriwa kuweka mboji katika shamba lako ili kuurutubisha udongo vizuri.

Utayarishaji wa kitalu na usiaji
Ni muhimu kusia mbegu katika trei ili kukwepa kupotea kwa miche pamoja na kupata miche bora. Miche huchukua siku saba hadi kumi kuchipuaa, na wiki tatu hadi nne kwenye kitalu, kisha kupelekwa shambani. Ikiwa mkulima atasia mbegu ardhini, ni vyema kuandaa eneo lenye mbolea ya kutosha. Waweza kuweka mbolea ya mboji katika eneo hilo au katika matuta yako uliyoyaandaa kwa ajili ya kusia mbegu.

Upandaji wa miche
Unapopeleka miche yako shambani, hakikisha unaotesha kwa kufuata maelezo muhimu ya utaalamu ili kuweza kupata mavuno mengi na yenye ubora. Matuta ya kunyanyua yasiyotuwamisha maji hushauriwa kutumika katika kilimo cha zao hili kwani huzuia kuoza kwa mimea maji yanapotuama. Nafasi kati ya mche na mche iwe sentimeta 60 huku nafasi kati ya mstari na mstari iwe ni hatua moja. Hakikisha shamba limemwagiliwa na weka mbolea ya mboji katika kila shimo wakati wa kuotesha.

Umwagiliaji 
Zao hili likipata maji ya kutosha husitawi vizuri hivyo ni muhimu kumwagilia mara mbili hadi tatu kwa wingi kulingana na msimu husika hasa wakati wa kiangazi. Usimwagilie kipindi cha mvua kwani utasababisha bilinganya kuoza kutokana na wingi wa maji.

Palizi 
Hakikisha unafanya palizi mara kwa mara na kuacha shamba likiwa safi wakati wote ili kuondoa ushindani wa magugu na mimea kwenye chakula, maji na mwanga. Pia kuzingatia usafi kutasaidia kupunguza kuzaliana kwa wadudu waharibifu pamoja na magonjwa.

Magonjwa na wadudu
Zao hili hushambuliwa na wadudu pamoja na magonjwa ya aina mbalimbali hasa linapolimwa wakati wa kiangazi. Utitiri: Wadudu hawa kwa kiasi kikubwa wamekuwa visumbufu vya zao hili na si rahisi kukuta bilinganya haijashambuliwa na wadudu hawa, hasa wakati wa joto au kiangazi.

Kimamba: Hawa wadudu pia hushambulia bilinganya mara kwa mara wakati wa kiangazi.

Inzi weupe (white flies): Wadudu hawa kwasasa ni visumbufu vya mazao mengi ya bustani ama ya mbogamboga, na bilinganya ni moja ya mazao yanayoshambuliwa na wadudu hawa kwa kiasi kikubwa. Bilinganya inapoanza kuzaa matunda, wadudu hawa huvamia na hujikita katika majani, hufyonza maji na hatimaye bilinganya hukauka. Wadudu hawa hueneza ugonjwa unaofahamika kwa jina la Rasta. Huweza pia kusababisha majani kubadilika rangi na kuwa meusi

Barafu: Huu ndio ugonjwa mkubwa unaosumbua zao la bilinganya, na mara nyingi ugonjwa huu hutokea kipindi cha mvua. Husababisha tunda ya bilinganya kupata ukungu, kuoza na kudondoka kwenye mti. Na inaposhika tunda moja, ni rahisi kuambukiza lingine kwa haraka na matunda ya mti wote hushambuliwa. Pia wadudu kama leaf miner, bollworm, beetle pamoja na magonjwa kama root rot, leaves sports, kutu, kuoza kwa tunda, bakajani hushambulia zao hili pia.

Namna ya kudhibiti
Wadudu huweza kudhibitiwa kwa kutumia mwarobaini, tumbaku, majivu na mafuta ya taa, majani ya mustafeli pamoja na mfoori kulingana na vipimo na namna ya utengenezaji kwa maelezo sahihi kutoka kwa mtaalamu wa kilimo. Ikiwa mkulima atatumia viuatilifu, ni muhimu kutumia kulingana na ushauri wa wataalamu. Pia kuepuka kulima zao hili katika msimu ambao wadudu hao wanakuwepo kwa kasi hasa kipindi cha kiangazi.

Mavuno 
Kwa wastani, bilinganya nyeupe hutoa kilogramu 10,000 hadi 15,000 kwa ekari moja. Aina hii ya bilinganya haina tofauti sana na aina nyingine kwani huchukua siku 80 hadi 95 kukomaa na kuanza kuvunwa. Kiwango cha mavuno huongezeka mchumo baada ya mchumo, kadri siku zinavyoendelea na pia kulingana na matunzo. Bilinganya hutoa mavuno mengi na bora kwa kipindi cha miezi mitatu mfululizo, baada ya hapo mavuno huwa hafifu.


Matumizi
Mboga hii hutumika kwa ajili ya kutengeneneza saladi japo wengine pia hutumia kama mboga au kama kiungo cha chakula.






“Kanitangaze” mdudu hatari kwa nyanya









Tuta absoluta (nondo) wanataga mayai usiku kwenye sehemu ya juu ya mimea, kwenye sehemu ya chini ya majani au shina changa au sehemu za maua. Katika maisha yao, mdudu jike huweza kutaga hadi mayai 260.


Wakulima wa nyanya nchini Tanzania na maeneo jirani, wameingiwa na hofu kubwa baada ya kuenea kwa haraka mdudu hatari anaeangamiza zao la nyanya. Mdudu huyo anayejulikana kama nondo wa nyanya, na kitaalamu Tuta absoluta, aligundulika kuwepo nchini tangu mwaka 2014, lakini madhara yake yameanza kuonekana zaidi mwaka huu na anaathiri uzalishaji wa nyanya kwa kasi na kiasi kikubwa sana jambo lilopelekea wakulima kumbambika jina la “kanitangaze”. Ni muhimu kwa wakulima kumtofautisha mdudu huyu na yule mwenye mapindo, ambae kwa kawaida hushambulia nyanya na mazao mengine. Wadudu wenye mapindo ni aina ya inzi-buu lake huzalisha kijumba chembamba, ambacho husukwa kwenye majani, lakini hakishambulii tunda kama ilivyo kwa Tuta absoluta. Tuta absoluta ni nondo na buu lake huzalisha vijumba vikubwa, ambavyo hushambulia tunda la nyanya na hatimae kusababisha hasara kubwa kwa mkulima.

Tabia za wadudu hawa 
Wadudu wakubwa wanafanya kazi usiku na mapema wakati wa asubuhi. Majira ya saa 1 hadi 5 asubuhi wanaweza kuonekana wakiruka kwenye sehemu ya juu ya mmea. Muda unaobaki wa siku wanajificha kwenye sehemu ya chini ya majani. Kwa kawaida huwa wanataga mayai usiku kwenye sehemu ya juu ya mimea, kwenye sehemu ya chini ya majani au shina changa au sehemu za maua. Katika maisha yao, mdudu jike huweza kutaga hadi mayai 260. Mayai yanapoanguliwa, mabuu hutumia masaa machache kujilisha juu ya mmea. Baada ya hapo, wanaingia ndani yam mea ambapo hukaa hadi wapevuke na kuwa wadudu wakubwa. Baadhi ya mabuu walio kwenye mabadiliko huondoka kwenye pango walilopo na kuanzisha jingine, wakati mwingine ni ndani ya tunda. Buu mmoja linaweza kuharibu tunda zima kwenye shada. Wakati mabuu wanapozunguka mmea, wanafanya haraka sana kwa msaada wa nyuzi nyororo walizotengeneza.

Ukuaji 
Ukuaji wa buu hufanyika kwenye udongo na kwenye mimea yenyewe. Mdudu anapopevukia kwenye mmea, hutengeneza kijumba chenye nyuzi laini ili kujilinda. Tuta absoluta ana uwezo wa kuwa na vizazi vingi katika kipindi cha miezi 12. Katika maeneo yenye joto, mzunguko unaweza kukamilika chini ya mwezi mmoja. Kutokana na muda wa mzunguko wa maisha kuwa mfupi, kuna hatua nyingi za mdudu huyu kuharibu mmea kwa kila kipindi kimoja cha maisha yake. Wadudu hawa hawapendi baridi kali wala joto kali sana. Chini ya nyuzi joto 10 inazuia ukuaji wa mdudu huyu, na zaidi ya nyuzi joto 30 hufa.

Uharibifu 
Wadudu hawa husababisha uharibifu enezi wa jani pamoja na tunda, ambao unaweza kusababisha hasara ya asilimia 100 kwa mkulima. Mimea ya nyanya inashambuliwa kuanzia hatua za awali, hadi inapotoa matunda. Uharibifu wa awali hupelekea hatua ya pili ya maambukizi ya kuvu na bakteria. Buu linaweza kushambulia tunda mara tu linapotengenezwa. Huharibu pia vichipukizi ambavyo husababisha ukuaji mbovu wa mmea. 

Udhibiti 
Kwa kawaida utunzaji wote wa mazao hutegemea maamuzi madhubuti na utunzaji sahihi wa shamba. Kwa upande wa utunzaji wa mazao, mdudu mharibifu anatakiwa asipate chakula kwenye mmea unaomhifadhi. 

Ili kudhibiti wadudu hawa, 
zingatia mambo muhimu yafuatayo: 
• Usipande tena mazao hifadhi mara tu baada ya uzalishaji wa mazao hifadhi ya mwanzo.

• Rudia kupanda mazao yasiyokuwa jamii ya mnavu 

• Unaweza kuacha eneo hilo kwa muda wa wiki 5 hadi 6 bila kuwa na mimea hifadhi. Hali hiyo itasaidia kuondoa kizazi cha wadudu hao katika eneo hilo 

• Ondoa magugu yote yenye majani mapana. Weka mkazo kwenye kuondoa magugu jamii ya mnavu

• Ondoa mara moja masalia ya mazao ya zamani, kisha yafukie 

• Ondoa nyanya zilizoharibiwa kutoka kwenye mmea na uziteketeze 

• Kuwa makini na utendaji wa majirani katika mashamba yao 

• Pangilia eneo lako vizuri kwa kuweka nafasi kutoka katika shamba la jirani 

Shughuli za binadamu 
Mdudu huyu anasambaa kwa haraka sana kutokana na shughuli za binadamu. Ni muhimu kufanya juhudi ili kuzuia uenezaji unaotokana na shughuli hizo. 

Tuta absoluta wanaweza kutaga mayai kwenye miche iliyopo kwenye kitalu. Hivyo kabla ya kutoa miche kwenye kitalu ni lazima ichunguzwe kwa umakini, ili kuona kama kuna dalili za wadudu waharibifu. 

Endapo wafanyakazi wamekuwa kwenye shamba lililozagaa wadudu, ni muhimu kuhakikisha kuwa hawabebi wadudu kwenye nguo zao kutoka eneo moja kwenda lingine. 

Hakikisha kuwa hakuna tunda lililoathiriwa na mdudu linalopelekwa sokoni. Tunda lililoharibika liteketezwe. 

Vikapu na matenga yanayotumika kuvunia kwenye eneo lililoathirika, visipelekwe kwenye eneo safi ambalo halijaathiriwa. 

Viuatilifu 
Kuna aina nyingi za viuatilifu vinavyoweza kuua aina hii ya wadudu- “Tuta absoluta” lakini kuna mambo mengi yanayowasaidia wasife kwa urahisi. 
• “Kanitangaze” Tuta absoluta, hujificha wakati wote. Anapokuwa mkomavu hujificha chini ya majani au mabuu ndani ya majani au tunda. Hali hii hufanya viuatilifu vya mguso au kunyunyiziwa kushindwa kuleta mafanikio. 

• Mdudu huyu hujenga uwezo wa kushindana na dawa zilizotumiwa kupita kipimo. 

Ili kuweza kukabiliana na mdudu huyu, ni muhimu sana kutumia kiasi kidogo sana cha viuatilifu kwa kuwa wana uwezo wa kujenga usugu kukabiliana na dawa hizo. Au kutumia dawa za asili zinazoaminika kuwa na uwezo wa kukabiliana na aina hiyo ya wadudu.