Total Pageviews

Sunday 21 February 2016

Wednesday 3 February 2016

Kilimo cha Maua



Ndugu Wapetani, kuna haja kubwa sana kwetu kuwa wabunifu na kuweza kuifanya biashara yetu hii kuwa yenye mvuto na tija kwetu.  Nasema haya kwa kuwa tumekuwa kama tumejisahau kidogo kwa kukaa na kusubiri wateja waje katika maeneo ya biashara zetu ili kutupa mia mbili mia tatu, tuna ishusha thamani biashara hii.  Hebu tutafute njia ya kulipendezesha jiji kwa kuingia mikataba maeneo mengi kwa ku design maeneo mengi na kuweka maua pamoja na miti,  tuandike miradi yetu na kuweka faida za kuwa na bidhaa zetu katika jiji hili la Dar es Salaam na Wilaya zake, tuwabadili fikra wakazi wa Dar kwa kuwa wekea mazingira mazur na si mabiwi ya takataka tunazoona na harufu mbaya tunayoinusa kila kukicha.  Ni wakati sasa wa kubadilika na kulitengeneza jiji.

Hivi ni lini mara ya mwisho umewaona vipepeo wazuri katika macho yako wakikatisha mbele ya macho yako zaidi ya inzi wa aina mbili, kama sio yule wa chooni , basi yule wa majalalani na katika vidonda na vinyesi anayetuletea magonjwa kama kipindupindu na maradhi mengine ya kijingajinga.

Tutumie fursa hii sasa ili kujiingizia kipato lakini pia kulipendezesha jiji.

Jiji la Dar tunaambiwa hakuna mashamba lakini tunaweza kuwa na mashamba ya maua na kuzalisha ajira kwa kulima, kuhifadhi na kuuza maua bila ya kuharibu taratibu za jiji.

Hii ni njia nzuri ya kuwavutia hata wadau na kuanza kuifanya hii biashara kuwa ajira, tena ajira yenye tija kwa wakulima kufanya biashara ndani na nje ya nchi.




Tuchukue mfano wa majirani zetu Kenya wao inakadiriwa zaidi ya Wakenya 500,000 wamejiajiri katika biashara hii, na wameajiri zaidi ya wafanyakazi 90,000 katika mashamba yao.

Mwaka 2013 tani zipatazo 125,000 za maua zilisafirishwa nje ya nchi na kuwaingizia kiasi cha dola za kimarekani 507 milioni ( kiasi cha shilingi za kitanzania 1,110,330,000,000/=) (Trilioni 1.1).

Kiasi cha 25.3% ya pato la Kenya hutokana na kilimo kwa ujumla, na kilimo cha maua kinachangia 1.3%

Wenzetu wakenya 35% ya maua, wanauza ulaya hasa nchi za Holland, Germany, UK, na nyinginezo.  Pia Kenya wana mashamba 127 yanayotambulika na kufanya biashara kimataifa.

Ni wajibu wetu wafanyabiashara wa kilimo hiki tuwe wbunifu na tushirikiane katika kuleta maendeleo yetu binafsi na ya taifa kwa ujumla.  Ukilitenga taifa kwa kutaka biashara iwe yako kama kisiwa hutapiga hatua zaidi ya kuishia kulaumu na kuona kama vile hii sio ajira yenye kuhitaji kulipwa mshahara mnono.

Twaweza jadiliana kwa wale wanaotaka tujiunge kwa pamoja na kuifanya biashara hii kuwa ajira rasmi itakayotuingizia kipato kikubwa kwetu na kwa taifa.  Jiunge nami kwa  WhatsApp namba +255765903379 FREBU Farm Group

JINSI YA KULIMA UYOGA NYUMBANI







Kabla ya kuzalisha uyoga inabidi kuwa na chumba chenye paa ambalo litazuia jua, mvua na vumbi.
Chumba hiki kinatakiwa kiwe na sakafu inayohifadhi unyevunyevu pamoja na sehemu ya giza ambayo ni muhimu kwa kuotesha utandoa wa Uyoga. Mkulima wa kawaida anaweza kutumia kasha kama sehemu ya giza.
Hatua muhimu katika kuotesha Uyoga baada ya kupata mbegu ni kama ifuatavyo;
Kusanya masalia ya mazao kama vile mabua, majani ya mpunga, ngano, pumba za mpunga au mahindi, masalia ya miwa baada ya kukamua n.k. Vitu hivi hutumika kama mali ghafi kwa kuoteshea Uyoga. Mabua, Majani ya Mpunga au Migomba yakatwe kwa urefu usiozidi sentimeta 6, au urefu wa vidole kwa kutumia panga au kisu.
Loweka mali ghafi kwenye maji ya kawaida kwa muda wa siku nzima ( saa 24). Kisha yachemshwe kwa muda wa saa 2 ili kuua vijidudu pamoja na vimelea vilivyomo. Ipua na umwage maji yote halafu tandaza kwenye kichanja kisafi ili yapoe bila kuchafuliwa na vumbi au vijidudu. Kisha jaza mali ghafi hii katika mifuko ya nailoni tayari kwa kupanda mbegu. 
Namna ya kupanda.
Kuna aina mbili za upandaji;

AINA YA KWANZA
Chukua mfuko wa nailoni, weka tabaka ya mali ghafi ya kuoteshea kiasi katika mfuko halafu tawanya mbegu juu yake. Baada ya kuweka mbegu, weka tena tabaka nyingine ya kuoteshea na kuweka mbegu juu yake.

Endelea kuongeza tabaka kwa namna hii mpaka ifikie ujazo wa robo tatu ya mfuko.
NB: Tabaka la mwisho la juu lazima liwe la vioteshea.

AINA YA PILI
Changanya mali ghafi ya kuoteshea ( baada ya kuchemsha na kupoa) na mbegu ya uyoga katika uwiano wa 1:25 ( mbegu : mali ghafi ya kuoteshea).Kwa uyoga aina ya Mamama (Pleurotus spp), kisha mchanganyiko huu ujazwe katika mifuko ya nailoni.

Mifuko hii iwe ya ukubwa wa sm 20 kwa sm 40 ambamo unaweza kujaza kilo 1-1.5 ya mali ghafi ya kutosha. Katika njia zote mbili, funga mifuko na toboa matundu kwenye mifuko yenye kipenyo cha sm 6 hadi 10 kwa kila mfuko. Zingatia:
(i) Matundu yawe mengi ili kuingiza hewa ya kutosha ndani ya mifuko.
Uyoga ni Kiumbe hai, hivyo unahitaji kupumua.
(ii) Ukishanunua mbegu, kama hupandi kwa muda huo, hifadhi kwenye jokofu. Kama huna jokofu, nunua mbegu baada ya kuandaa kila kitu.
Mbegu za uyoga zinaweza kuota vizuri hata zikikaa nje ya jokofu kwa siku mbili.
(iii) Waweza kutumia chupa moja yenye ujazo wa mililita 300 kwenye kilo 15 za mali ghafi ya kupteshea.
Hakikisha unamaliza mbegu yote kwenye chupa kwani ikibaki itapata maambukizo ya vimelea.
(iv) Hakikisha unaponunua mbegu iwe ni nyeupe. Mbegu ambayo siyo nyeupe ni dalili za maambukizo ya vimelea. Vingine na hivyo haifai kupandwa .

MATUNZO YA ZAO LA UYOGA.
Weka mifuko kwenye chumba cha giza. Kwa mkulima wa kawaida waweza kutumia kasha lisilopitisha mwanga kama chumba cha giza. Acha mifuko humo kwa muda wa siku 14-21 bila kufunua ili ukungu mweupe uweze kutanda vizuri. Utando wa uyoga ukishatanda vizuri kwenye mali ghafi ya kuoteshea, hamishia kwenye chumba cha mwanga na hewa ya kutosha kisichopigwa jua.
Katika chumba chenye mwanga. Mifuko inaweza kuwekwa kwenye meza, chanja ya waya au miti.
Mifuko pia inaweza kuning'inizwa kwenye kamba.

NB: Unaweza kunyunyizia maji juu ya mifuko yaliyochemshwa na kupoa, mara tatu au zaidi kwa siku.

Tahadhari: Usizidishe maji kwani maji yakiwa mengi sana yanaweza kuozesha uyoga.

Aina nyingi za uyoga huanza kutoa vichwa siku 2-3 baada ya kuwekwa kwenye mwanga.

UVUNAJI WA UYOGA.
Uyoga huwa tayari kuvunwa siku tatu baada ya vichwa kuonekana. Uyoga uvunwe kwa mkono kwa kushika katikati ya shina la uyoga, kisha zungusha hadi uyoga ung'oke. Usiondoe kichwa peke yake katika kuvuna uyoga kwa kubakiza shina huzuia uyoga mwingine kutokea.

Nakutakia mafanikio katika kilimo 

Je Wajua kuwa Uyoga ni Kinga ya Saratani?
Uyoga una vitamini na aina nyingi za madini.
Virutubisho vilivyothibitishwa kuwemo kwenye uyoga ni pamoja na Vitamin B2, B3, B5, B6, B Complex pamoja na madini ya Potasiamu na ‘phosphorus’.
Virutubisho hivyo ni muhimu
kwenye mwili wa binadamu katika kutoa na kuimarisha kinga ya kupambana na ‘wavamizi’ maradhi.
Aidha,
inaelezwa kuwa uyoga ni chanzo kingine kizuri sana cha madini ya chuma (iron) na kopa ambayo yanahusika kwa kiasi kikubwa na uwezeshaji wa usambaza wa hewa ya oksijeni mwilini. Kupatikana kwa madini ya chuma na kopa kwenye uyoga ni jambo la kipekee ambalo linafanya mmea huo kuwa tofauti na muhimu.
Nguvu za uyoga 
(Mashrooms) kwa mapana, inaelezwa kuwa Vitamin B2 inayopatikana kwenye uyoga, ni tiba tosha kwa watu wanaosumbuliwa na ugonjwa wa kichwa unaojulikana kama ‘kipanda uso’. Kiasi kidogo cha uyoga utakachokula kitapunguza kasi ya kuumwa kichwa hicho.
Vitamin B
inasifika kwa uwezo wake wa kuzuia uchovu wa mwili (fatique) na akili hasa wakati wa kazi nyingi. Vitamin B3 husaidia kupunguza kiwango cha mafuta mabaya ya Lehemu mwilini, wakati Vitamin B6 yenyewe huondoa hatari ya mtu kupatwa na kiharusi au moyo kusimama ghafla (Heart Attack).
Faida za kiafya zilizo orodheshwa hapo juu zinazopatikana kwenye uyoga hazikutosha, basi kuna faida nyingine ambayo inatokana na madini aina ya Zinc yanayopatikana kwa wingi kwenye mboga hii. Zinc ina faida nyingi sana mwilini na miongoni mwa faida hizo ni uimarishaji wa kinga ya mwili (Immune System).
Zinc si muhimu tu kwa uimarishaji wa kinga mwilini, bali pia kwa uponyaji wa haraka wa vidonda mwilini. Vilevile mboga hii inasaidia sana ukuaji mzuri wa seli za mwili, huimarisha kiwango cha sukari mwilini na kukufanya kusikia ladha na harufu ya vyakula na vitu vingine ipasavyo.
Kwa ujumla uyoga ni mboga muhimu na inapaswa kuliwa na kila mtu anayejali afya yake kutokana na faida zinazopatikana humo. Kuanzia leo, jaribu kuweka uyoga katika orodha ya mboga unazonunua kila wiki kwa ajili ya familia yako.